Siku moja baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa Maji wa Same -Mwanga- Korogwe Septemba 24, 2021, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba ametembelea eneo la usambazaji wa mabomba ambalo linatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Ziara hiyo ameifanya Septemba 25, 2021 akiambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Wizara hiyo CPA. Joyce Msiru
Mhandishi Kemikimba akizungumza baada ya kukagua kazi hiyo amesema ameridhishwa na hatua ya utekelezaji inayoendelea na DAWASA.
"Baada ya kutembelea maeneo yote, nimeridhika na jitihada zinazofanywa na DAWASA. Nafahamu kuwa moja ya agizo la Mhe. Waziri Mkuu ni kuhakikisha vijiji ambavyo tulikuwa hatujaanza utekelezaji vikiwemo vinavyozunguka eneo la chanzo cha maji tunavifikia ili maji yakianza kutoka, na wao wapate huduma. Nawahakikishia wananchi kuwa kazi hiyo tutaifanya kwa haraka bila kuchelewa." Mhandisi Kemikimba amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi DAWASA Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema utekelezaji wa mradi huo unakwenda vizuri.
"Katika eneo la Mwanga tulitakiwa kusambaza mabomba kilometa 53, tumeshasambaza Kilometa 49. Upande wa Same tumesambaza kilometa 3 kati ya 15. Lengo ni kukamilisha kilometa zilizobaki mwishoni mwa mwezi Oktoba 2021." Mhandisi Mtindasi amesema.
Amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya wakati.
Mradi wa Same - Mwanga-Korogwe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 262 na unatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya laki nne.
Ещё видео!