Hoja ya utekaji, mauaji na kupotea kwa watu ikiwemo watoto imeibuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest kutaka mkakati wa Serikali kukomesha matukio hayo aliyodai baadhi yanahusishwa na vyombo vya dola.
Leo Alhamisi, Agosti 29, 2024, hoja hiyo imeibuka bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, baada ya Anatropia kusema matukio ya utekaji, mauaji na kupotea kwa watu yanaashiria uvunjifu wa haki za binadamu.
Amesema matukio hayo yamekuwa na sura tofauti tofauti ikiwemo wivu wa mapenzi na ushirikina.
“Lakini na matukio mengine ya kutekwa na kupotea kwa watu yanahusishwa na vyombo vya dola. Nataka kufahamu mkakati wa Serikali kuzuia matendo haya lakini kuondoa taharuki ambayo inajitokeza katika jamii,” amesema.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kabla ya kumpa nafasi Majaliwa kulijibu swali hilo, amesema juzi Jumanne Agosti 27, 2024 alisimama Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani akazungumzia suala hilo.
Amesema mambo hayo yanayohitaji uchunguzi:“Leo asubuhi nimesoma kuna mganga amezika watu sijui 10 na ngapi, sasa huyu mganga ni polisi ambaye watu ameuawa na wamezikwa kwake.”
Amesema mambo hayo yakiwa yanasemwa kwa hisia hivyo inakuwa kama mtu hajali wakati kila mtu anajali na kila binadamu ana haki ya kuishi.
“Lakini tusiweke mazingira kwamba kila anayepotea…si kuna mabasi wanapanda kule chini, akidondoka huko chini si nyumbani wanamtafuta utasema ni chombo cha dola kimemchukua.Sisi lazima tuifanye hii kazi kama viongozi ukichukua mihemko hutoi nafasi kwa Serikali kufanya kazi yake wakati huo huo hutoi nafasi kwa jamii kuendelea kushiriki katika jambo,” amesema.
Amesema wao wote ni viongozi na wangependa wananchi wao wawe salama na kuonya mambo hayo yasichukuliwe jumla jumla.
“Na wewe chukua nafasi ya uongozi, unaweza kutoa ushauri lakini usinyooshe vidole kwa sababu huna hakika. Na wengine wanahama nchi si tunakamata hapa kila siku, na wenyewe huko kwao wanatafutwa watasema chombo cha dola kimewachukua kimewapeleka sijui wapi,” amesema.
Amesema huku kwao wanawatafuta wahamiaji hao waliokamatwa nchini lakini kumbe alipofika hapa Tanzania mazingira yamekuwa magumu na hivyo amekamatwa.
Baada ya maelezo hayo ya Spika Tulia, amempa nafasi Waziri Mkuu Majaliwa kueleza akisema jukumu la kulinda nchi ni wajibu wa Watanzania wote kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama vyenye jukumu la kupokea taarifa mbalimbali zinazoonyesha uvunjifu wa amani popote pale kwenye meza ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Jukumu lao baada ya kupokea taarifa ni kuhakikisha wanafanya uchunguzi,” amesema.
Majaliwa amesema uchunguzi unapobaini waliotenda makosa, wanawapeleka katika vyombo vya sheria.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kujikita kusimamia misingi ya amani katika nchi yetu na usalama kwa kuhakikisha raia na mali zao zinabaki salama.
Amewahakikishia Watanzania kwamba suala la ulinzi na usalama bado liko mikononi mwao pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
“Jukumu letu ni kuhakikisha tunasaidia vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa zozote zile ambazo zinaleta tishio la amani ili kuvisaidia vyombo vyetu viweze kuchukua tahadhari na hatua stahiki ili kubaini watu wote wanaotishia kutokuwepo kwa amani katika nchi yetu,” amesema.
Majaliwa amesema lakini pia vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na wajibu wao wa kuhakikisha kila taarifa inayopatikana lazima ifanyiwe uchunguzi na kubaini wale wote wanaohusika na kama wanapatikana wachukuliwe hatua mara moja.
Amemshukuru Spika kwa maelezo yake ya awali ili kuondoa upotoshaji ambao unaweza kuwa unaendelea na kufanya vyombo vyao vishindwe kufanya kazi yake na kuwavunja moyo watu wanaofanya kazi saa 24 kwa ajili ya ulinzi ambao unawafanya wabaki salama.
MaRC na DC tena bungeni
Katika swali jingine, Mbunge Viti Maalumu, Stella Fiyao amesema nchi inaamini katika uongozi wa kisheria na utawala bora ili kujengwa umoja mshikamano na upendo baina ya wananchi na viongozi wao.
Amesema hata hivyo kumekuwa na changamoto kubwa baina ya baadhi ya wateule wa Rais, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kwa kutumia nguvu na mamlaka yao vibaya kukamata viongozi na wananchi na kisha kuwatupa ndani.
“Moja jambo hili limetengeneza chuki kubwa baina ya wananchi na Serikali yao lakini linafifisha jitihada kubwa za mheshimiwa Rais za kuhubiri 4R na mwisho wa siku jambo hili linakuwa halileti mantiki,” amesema.
Ametaka kujua kauli ya Serikali ni ipi katika kukemea jambo hilo ambalo linatengeneza chuki kubwa baina ya Watanzania na Serikali yao.
“Kauli ya Serikali ni ipi kwa hawa viongozi wanaotumia mamlaka yao kutesa na kunyanyasa wananchi,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema swali hilo ni linafanana na alilolisema jana Jumatano Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi ambapo Dk Tulia aliwapa kazi Serikali kulifanyia kazi.
Ещё видео!