Zaburi 91
Mungu mlinzi wetu
1Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu,
anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu,
2ataweza kumwambia Mungu:
“Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu;
Mungu wangu, ninayekutumainia!”
3Hakika Mungu atakuokoa katika mtego;
atakukinga na maradhi mabaya.
4Atakufunika kwa mabawa yake,
utapata usalama kwake;
mkono wake utakulinda na kukukinga.
5Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku,
wala shambulio la ghafla mchana;
6huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku,
wala maafa yanayotokea mchana.
7Hata watu elfu wakianguka karibu nawe,
naam, elfu kumi mkono wako wa kulia,
lakini wewe baa halitakukaribia.
8Kwa macho yako mwenyewe utaangalia,
na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa.
9Wewe umemfanya Mungu kuwa kimbilio lako;
naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako.
10Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote;
nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote.
11 Maana Mungu atawaamuru malaika zake,
wakulinde popote uendapo.
12 Watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa kwenye jiwe.
13 Utakanyaga simba na nyoka,
utawaponda wana simba na majoka.
14Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye;
nitamlinda anayenitambua!
15Akiniita, mimi nitamwitikia;
akiwa taabuni nitakuwa naye;
nitamwokoa na kumpa heshima.
16Nitamridhisha kwa maisha marefu,
nitamjalia wokovu wangu.”
Ещё видео!