Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Simbayao ambaye ni miongoni mwa maofisa watatu walioshambuliwa na wananchi Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam wakati akitaka kukamata gari linalodaiwa kuingizwa nchini kimagendo, amefariki dunia.
Taarifa za kifo chake zimetolewa leo usiku Ijumaa Desemba 6, 2024 na mamlaka hiyo kupitia taarifa kwa umma iliyopochapishwa katika mitandao yake ya kijamii.
“Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inasikitika na kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kutokana na kifo cha mtumishi wetu wa TRA, Amani Kamguna Simbayao kilichotokea leo mchana wa Desemba 6, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa baada ya tukio la shambulio akiwa katika majukumu yake ya kikazi kwa masilahi ya Taifa katika eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam.
Pia katika taarifa hiyo TRA imesema: “Tunatarajia wahusika wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.”
Tukio hilo la kushambuliwa kwa ofisa huyo akiwa na wenzake wawili lilitokea usiku wa Desemba 5, 2024 wakati watumishi hao wakiwa kwenye gari la Serikali.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameonya vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Ещё видео!