Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana ni tukio linalotukumbusha na kututafakarisha pia kuhusu ubatizo wetu sisi wenyewe. Mwinjili Marko amesisitiza mambo yale yaliyotokea baada ya ubatizo wa Yesu: mbingu kufunguka, Roho kushuka kwa mfano wa njiwa na sauti kusikika kuwa “wewe ni mwanangu mpendwa ninayependezwa nawe”. Ubatizo: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu.
Na Padre William, Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Dominika inayofuatia sherehe ya Epifania, yaani Tokeo la Bwana, Kanisa huadhimisha sherehe ya Ubatizo wa Bwana. Sherehe hii ya Ubatizo wa Bwana ndilo adhimisho linahitimisha kipindi cha Noeli na kuashiria kuanza kwa kipindi cha kawaida cha liturjia katika Mwaka wa Kanisa. Kwa adhimisho hili ni kama vile tunahama sasa kutoka kuadhimisha kuzaliwa na utoto wa Yesu kuanza saa kuadhimisha utume ambao Yesu ameufanya. Ubatizo wa Yesu unakuwa ni kiashirio kwamba wakati wake umefika, wakati wa kuanza kuutekeleza utume wake. Karibu ndugu msikilizaji na msomjaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu kwa sherehe hii ya Ubatizo wa Bwana. Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Is 55:1-11). Katika somo hili la kwanza, Nabii Isaya anatoa mwaliko wa kuupokea wokovu. Isaya anatoa mwaliko huu kwa wana wa Israeli waliokuwa utumwani Babeli na wokovu anaowatangazia ni kuwa hali yao ya utumwa itaisha na watarudishwa katika nchi yao. Anatumia lugha ya picha kuuelezea wokovu huo ambao kimsingi ni Mungu mwenyewe ndiye anayeutoa.
Na lugha anayotumia ni ile lugha ya wachuuzi au ya wafanya biashara katika masoko au minada tuliyoizoea. Anasema “kila aonaye kiu aje anywe, kila asiye na fedha na aje. Njooni mnunue divai na maziwa bila fedha na bila thamani kwani haifai kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula”. Kwa lugha hiyo, Isaya anaonesha kuwa mwaliko anaoutoa ni mwaliko unaohitaji mwitikio wa haraka. Ni bure kwa maana kwamba hauna gharama na hivyo haumpi mzigo wowote yule anayealikwa. Tunaona kwamba huu ni mwaliko wa wokovu kwa sababu maneno “kula na kunywa” au wakati mwingine inapotamkwa “karamu” ni maneo ambayo kibiblia yanaashiria wokovu na furaha ya kukutana na Mungu na kushibishwa mema yake. Na wale walio na “njaa na kiu” ndio wale wahitaji wa wokovu huo. Isaya anapowaonywa kuwa “kwa nini kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula” anawaonya wasihangaikie mambo yasiyo ya maana kwao, wasiweke tumaini lao katika yale yasiyoweza kuwasaidia na wasiwasikilize wale ambao mwisho wa siku watawahadaa.
Waisraeli wakiwa huko utumwani Babeli, waliibuka pia manabii wa uongo. Wengine waliwakatisha tamaa kwamba hawatakaa warudi makwao na wengine kuwajaza hofu na kuwatangatangisha kiimani. Onyo analolitoa Isaya ni kwa watu hawa waliojaa hofu na wanaotangatanga kiimani kuwa wokovu wa Mungu upo na ni wa uhakika. Ahadi zake ni za kweli na Neno lake ni lazima litimie. Isaya anawaalika watulie katika imani yao, waendelee kumtumainia Mungu na waupokee mwaliko wake wa wokovu. Somo la Pili (1Yoh 5:1-9): Somo hili linatoka katika Waraka wa Mtume Yohane kwa watu wote. Mwanzoni kabisa mwa waraka huu, Yohane anaeleza kuwa ameuandika ili kuwahubiria watu habari za Neno la Uzima kwa lengo la kuwapa uhakika wa kuupata uzima wa milele. Katika somo la leo anaeleza sasa kuwa hilo Neno la Uzima analohubiri ni Yesu Kristo ambaye amezaliwa na Mungu. Ndiye aliyekuja ulimwenguni katika maji na damu, yaani kwa kuutwaa ubinadamu halisi. Kuwa na imani kwake ni kuushinda ulimwengu na kuushinda ulimwengu ndio kuupata uzima wa milele.
Tafadhari Subscribe, Like, Comment na Share tone hili la upendo kwa ndugu jamaa na marafiki.
Jumuika nasi katika mitandao mingine ya Kijamii:
Instagram: [ Ссылка ]
Facebook: [ Ссылка ]
Mawasiliano:
JUGO MEDIA,
Sokoine Drive, Posta
P. O. BOX 34014,
Dar es Salaam.
For Bookings and other Enquiries
Phone Number +255757560764/657790405
#jugomedia #kanisakatoliki #familiatakatifu #wawata #uwaka #viwawa
Ещё видео!