Mwiba Mdogo sehemu ya 12
ILIPOISHIA JANA...
“...Mitego yake ukiiangalia vibaya utaiona ya kitoto, lakini imetegwa kwa akili kubwa sana, yataka utulivu wa hali ya juu,” alisema Maliki huku akifungua dirisha na kuchungulia nje. “Mkuu alitumia kama kuning’inia kutoka juu.”
ENDELEA...
“Muuaji ni mtu makini sana ambaye ana hesabu hatua zetu, tukitoa mguu yeye anakanyaga,” Chifu alisema.
“Lazima nimpe hongera zake, japo siamini anayefanya mauaji haya si huyo binti, bali mtu mwingine kabisa mwenye uzoefu na mauaji ya hesabu kali,” Queen aliongezea.
Wakiwa katikati ya mazungumzo Chifu Shila alikumbuka kukutana na Mtoto wa Marehemu.
“Jamani Mtoto wa Marehemu amepanga tuonane wakati huu ili tujue sababu ya yeye kufanya mauaji japokuwa inaonekana ni kisasi cha kuuliwa wazazi wake, pia kudhulumiwa pesa baada ya kuuza madini kwa kugawiana watu watano na mmoja kumtosa.
“Kuna imani tutajua sababu ya kifo cha baba na mama yake, pia uwezo mkubwa wa kijasusi ameupata wapi.”
Kabla ya uondoka alimpigia simu Mtoto wa Marehemu ambaye alipokea bila hofu yoyote ilionyesha anajiamini kupita kiasi kwa kuzungumza kwa kujiamini.
“Upo wapi binti yangu?”
“Nipo hapa ofisini mapokezi nakusubiri.”
“Sawa nakuja.”
“Vipi yupo wapi?” Maliki aliuliza.
“Yupo ofisini anatusubiri.”
“Mmh! Ni mtu wa aina gani anayejiamini kupita kiasi, natamani kumuona,” Queen alisema kwa shauku kuu.
Gari lilielekea makao makuu ya polisi, walitumia dakika kumi kufika.
Walipofika waliteremka na kuelekea ofisini, huku kila mmoja akiwa na shauku kumuona mgeni wao.
Walipofika mapokezi Chifu alishtuka kumuona binti yake ambaye alipotezana naye katika mazingira ya kutatanisha. Hakuwa binti yake wa kumzaa, bali rafiki kipenzi wa mwanaye Rashila ambaye kwa kipindi kile alikuwa mwanasheria wa kampuni ya mawasiliano.
Alishtuka kumuona amekaa pale lakini akili yake ilikuwa kwa mgeni wake, Mtoto wa Marehemu.
Ещё видео!