RUSSIA imekanusha madai kwamba huenda ajali ya ndege ya Shirika la Azerbaijan Airlines namba J2-8243, imetokea baada ya kudunguliwa na mfumo wa kujilinda wa anga wa taifa hilo.
Ndege hiyo ya Azerbaijan ilipata ajali juzi Jumatano Desemba 25, 2024, ikitokea jijini Baku, Azerbaijan kwenda Grozny Chechnia nchini Russia, hata hivyo, haikufakiwa kutua baada kupata hitilafu na kulazimika kwenda kutua kwa dharura katika uwanja wa Aktau nchini Kazakhistan.
Jitihada za kutua kwa dharura nazo hazikufanikiwa, badala yake ilidondoka takriban kilometa tatu kutoka ulipo uwanja wa Aktau na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 38 huku wengine 29 wakiokolewa wakiwa hai.
Baada ndege hiyo kupata hitilafu ikiwa kwenye anga la Russia, vyombo mbalimbali vya habari na mataifa mengine yaliibua tuhuma kuwa mwonekano wa mabaki ya ndege hiyo yanaashiria kuwepo matundu yanayodhaniwa kuwa ya risasi. Matundu hayo yakadaiwa kuwa ilishambuliwa ilipofika kwenye anga la Russia.
Mkuu wa Kitengo cha Anga cha Russia, Dmitry Yadrov, akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa Desemba 27, 2024, amesema mifumo ya kujilinda ya anga la Russia ilikuwa imezimwa hata kabla ndege hiyo haijagusa anga la Russia.
Badala yake, Yadrov amesema wakati huo Droni za Ukraine zilikuwa mguu sawa kufanya mashambulizi dhidi ya Russia huku akigoma kuzungumzia uchunguzi wa madai ya kuhusika na shambulio hilo.
Hata hivyo, kampuni ya ndege hiyo, ilidai kwamba ajali ya ndege hiyo ilitokana na mwingiliano wa kiteknikali katika mifumo ya anga na kwenye uwanja wa ndege ilipotarajiwa kutua japo haikuweka wazi ni wapi mwingiliano huo ulitokea.
Kwa mujibu wa manusura wa ajali hiyo, kabla ndege hiyo haijaanguka, walisikia sauti ya nguvu zikikita kwenye bodi la ndege hiyo ilipokuwa ikikaribia anga la eneo la Grozny.
Mhudumu wa ndege hiyo, Aydan Rahimli alisema baada ya kishindo hicho cha kelele kusikika, vifaa vya oksijeni vilifunguka, jambo lililomlazinu kwenda kutoa huduma ya kwanza kwa mhudumu mwenzake, Zulfugar Asadov, ghafla wakasikia imegonga ardhini.
Kwa upande wake, Asadov alipohojiwa akiwa hospitalini alisema alisikia sauti kama ya kitu kikikita kwenye bodi la ndege hiyo huku akikanusha kuwa vifaa vilivyobeba oksijeni kuwa vililipuka.
Madai ya ndege hiyo kushambuliwa yamekaziwa na Waziri wa Usafirishaji wa Azerbaijani, Rashad Nabiyev ambaye alisisitiza kuwa ndege hiyo imedunguliwa ikiwa kwenye anga la Grozny, Chechnia nchini Russia.
Hadi sasa mamlaka nchini Russia, Azerbaijan na Kazakhstan zinasubiria kusikia majibu ya uchunguzi wa wataalamu kuhusiana na kisa cha ndege hiyo kudondoka.
Pamoja na hatua hizo, Mbunge wa Azerbaijan, Rasim Musabekov, amedai kuwa kuanguka kwa ndege hiyo ni matokeo ya mashambulizi huku akiitaka Russia kuomba radhi kwa kitendo hicho.
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Musabekov, Msemaji wa Ikulu ya Kremlin nchini Russia, Dmitry Peskov amekanusha madai hayo na kusema wenye ukweli ni kamati zilizoundwa kuchunguza sakata hilo.
“Tukio la ajali hiyo linachunguzwa na hatuoni kama tuna haki ya kuanza kuhukumiana hadi pale ripoti ya wataalamu itakapoanikwa,” amesema Pescov.
Hata hivyo, Yadrov, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Anga cha Russia amesema ndege hiyo ilipokaribia kutua mifumo ya ulinzi wa anga ilizimwa kutokana na ongezeko la ukungu kuzunguka uwanja huo wakati ambao Droni za Ukraine zilikuwa mguu sawa kuishambulia Russia.
“Hali iliyokuwepo katika uwanja wa Grozny ni ngumu kwa ndege kutua ndiyo maana unahitajika uchunguzi unaohusisha pande zote,” amesema ofisa huyo.
Tovuti ya masuala ya anga ya FlightRadar24 ilichapisha taarifa kuwa ndege hiyo kabla ya kuanguka ilipata hitilafu katika mfumo wake wa Rada na kudai mfumo huo wa rada unadaiwa kuathiriwa na mifumo ya kujilinda ya Russia.
Kutokana na ajali hiyo baadhi ya safari za ndege zimeahirishwa kwenda Grozny nchini Russia ikiwemo kampuni ya Qazaq Air, na FlyDubai ambayo ilikuwa na safari leo kutokea Mji wa Sochi kwenda Mineralnye Vody kusini wa Russia hadi Januari 5, mwakani.
IMEANDIKWA NA MGONGO KAITIRA KWA MSAADA WA MASHIRIKA.
Ещё видео!