Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mh Ummy Mwalimu tarehe 15/05/2021 amekutana na wananchi zaidi ya mia moja wanaolalamika kutolipwa fidia ili kupisha ujenzi wa barabara ya Tanga Pangani.
Katika mkutano wa wazi uliofanyika shule ya Sekondari Mwapachu iliyopo Mwakidila wananchi hao walieleza kutoridhishwa na maelezo waliyopewa na TANROADS Mkoa wa Tanga kuwa hawapaswi kulipwa fidia kwa kuwa wao wameifuata barabara hivyo Sheria haiwatambui isipokuwa watu 31 tu.
Wananchi hao akiwemo Mzee Ombeni Elitwaza Ngoda, Mzee Mwihaji Zumo Mwihaji na Mohammed Juma Mjaruba wameeleza kuwa watu 117 hawakubaliana na maelezo hayo ya TANROADS kwa kuwa mwaka 2013 wote waliwekea alama ya X na baadae walifanyiwa tathmini, kupigwa picha na kufungua akaunti kwa ajili ya kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo. Aidha wameeleza kuwa mbona watu watakaopisha ujenzi wa barabara kuanzia Pangani - Bagamoyo wote wanalipwa iweje wa Tanga Pangani tu ndio wasilipwe?
Baada ya kusikiliza kilio hiki, Mheshimiwa Mbunge alisema akiwa mwakilishi wao amepokea kilio chao, majonzi yao na simanzi yao na kuwa yupo nao bega kwa bega kuhakikisha haki yao inapatikana. *Mhe Ummy alipendekeza kwa wananchi hao kuteua wawakilishi 5 ili kwenda nao Dodoma kupeleka kilio hiki kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mh Leonard Chamuriho*. Pendekezo hilo lilipokelewa kwa shangwe na wajumbe wote na hivyo sasa taratibu za safari ya kwenda Dodoma zimeanza ambapo gharama za nauli, chakula na malazi kwa wawakilishi watano zitalipwa na Mbunge.
![](https://i.ytimg.com/vi/jbwM0DaS6F0/maxresdefault.jpg)