Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ni jambo lisilokubalika kwa Mamlaka kuvunja Sheria, ikiwemo kuteka na kuua watu wasiokuwa na hatia, hata iwapo ni watuhumiwa.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT-WazalendoTaifa, ameyasema hayo leo Disemba 26, 2024, alipokua akitoa Mkono wa Pole kwa Familia za Marehemu Amour Salim Khamis (28) wa Kijiji cha Chonyi, na Othman Hamad Othman (75) wa kijiji cha Kimango, wote wa Kiungoni, Jimbo la Pandani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema hakuna Sheria inayoruhusu Dola au Mamlaka yoyote, kumshika au kumteka Raia hai na huru, na kisha mara tu kumrudisha akiwa maiti, hata iwapo anatuhumiwa kutenda kosa lolote.
Amesema kwamba iwapo kuna pahala pamekuja kutonesha majeraha ya muda mrefu, hasa katika Maeneo hayo ya Kiungoni na Vijiji vya Jirani, ni Tukio la Mauaji ya Watu hao.
"Na katika hili kuna Sheria; na iwapo Mtu akituhumiwa kwa jambo lolote; muuaji awe ni Askari, awe ni yoyote, hakuna aliyeko juu ya Sheria; ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha kila ambaye anahusika na hili, lazima Sheria ichukue mkondo wake", amesema.
Mheshimiwa Othman amefahamisha akisema, "haya yametokea kwa sababu utu umeondoka; hata ingelikuwa wametenda kosa kubwa la uhaini, basi haendi tu kuuliwa, bali lazima kwanza utaratibu ufuatwe, hadi mhusika atiwe hatiani".
"Wajibu mkubwa wa Mamlaka za Serikali ni kusimamia Haki, Sheria na Utulivu, haiwezekani tu Mtu ajichukulie Sheria mkononi mwake, hata akiwa ni nani", ameongeza Mheshimiwa Othman.
"Sasa inakuwaje mtu ambaye hata hajatiwa hatiani, achukuliwe na auliwe tu; hili hatuwezi kulinyamazia kimya", ameendelea kuhoji Mheshimiwa Othman huku akiahidi kusimamia kadhia hiyo.
"Hapa nataka niwaahidi, sisi kama Serikali ni wajibu wetu ni dhamana yetu kusimamia Sheria za Nchi, na tuliapa kwa kushika Kitabu cha Mwenyezi Mungu", amefahamisha Mheshimiwa Othman, akiahidi kufuatilia na kusimamia Kadhia hiyo hadi haki itendeke.
Aidha, amewahimiza Wana-familia, Ndugu, Jamaa, Marafiki, pamoja na Wananchi, kuwa na subra, hasa katika kipindi hiki kigumu cha msiba, uliotokana na na Mauaji ya Watu hao.
Kwa upande wake, Muwakilishi wa Jimbo la Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad ameeleza, yeye na Wananchi wake, wamesikitishwa mno na kitendo cha Mauaji ya Watu hao wasiokuwa na hatia.
Msiba wa Watu hao, wanaoaminika kufariki baada ya kuchukuliwa Majumbani kwao, umetokea juzi Disemba 24, huko Maeneo ya Pujini, kabla ya Maiti zao kupatikana huko Chake Chake Pemba.
Wakieleza masikitiko yao mbele ya Mheshimiwa Othman, Baba wa Marehemu Amour, na Kaka wa Marehemu Othman, Mzee Salim Khamis, na Mzee Salum Hamad Othman, wameitaka Serikali kufuatilia Kadhia hiyo kwa uadilifu, na kuhakikisha haki inatendeka, pamoja na kuwawajibisha wote waliohusika kusababisha Mauaji hayo.
"Mimi mnaniona sikuweza kuyasema haya tangu juzi, sinyamazi kulia, na nimemuomba Mwenyezi Mungu Anijaalie niweze kuyasema hapa Alhamdulillahi; hatujafahamu kisa na sababu ya Mwanangu mdogo, ninategemea anisaidie katika maisha, leo achukuliwe arudi Maiti; mie si radhi Duniani na Akhera, kama Serikali haijachukua hatua katika hili", amesema Mzee Salim, Baba wa Marehemu Amour.
Mzee huyo, akiongea kwa hisia za uchungu na masikitiko ameongeza kwa kusema, "tunaambiwa si ruhusa kujichukulia sheria mkononi, mbona hawa wao waajichukulia sheria mkononi kwa kutuulia watoto wetu wasio na hatia".
"Kweli Mheshimiwa tunakuomba Jambo hili ulisimamie, na Mungu Atakupa Uwezo, lakini na hili haki itendeke, ili kila mhusika aliyeshiriki kutenda dhulma hii awajibishwe; waliwaua tu hawakuwa wamefanya kosa wala kitendo chochote", ameongeza
Viongozi mbali mbali wameungana na Mheshimiwa Othman katika Ziara hiyo, wakiongozwa na Mratib wa Chama kisiwani Pemba, Ndugu Rashid Ali Abdallah; na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo wa Mkoa wa kichama wa Wete, Ndugu Juma Khamis Ali, pamoja na Wawakilishi wa Majimbo ya Mtambwe na Wingwi.
Katika Ziara hiyo, Mheshimiwa Othman aliketi na kuwafariji Wafiwa na Jamaa wa Marehemu, pamoja na Wanafamilia, kwa mida na mahala tofauti, ikiwemo ndani ya Madrasat Juhudiya, na Madrasat Hidayatil Atfaal, zote za Kiungoni Chonyi na Kimangu, Vikao ambavyo vimejumuisha Dua iliyoongozwa na Sheikh Maarufu wa Hapo, Maalim Hamad Juma Hamad.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Disemba 26, 2024.
Ещё видео!