Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, Christina Nindi (56) aliyeuawa kwa kupigwa risasi.
Taaifa za awali zilieleza tukio hilo lilitokea Novemba 12, 2024 katika Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, Wilaya ya Kilolo alipokuwa akiishi baada ya kushambuliwa, kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospita ya Rufaa ya Tosamaganga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili, Desemba 15, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi amesema uchuguzi wa tukio hilo unaendelea na mpaka sasa wamekamatwa watuhumiwa kadhaa, huku wengine wakiachiwa baada ya kubainika hawakuhusika.
“Kuna baadhi ya watuhumiwa tuliachia baada ya kubainika hawakuhusika, lakini hadi sasa tuna watuhumiwa watatu bado tunawashikilia na uchunguzi dhidi yao unaendelea. Tupo hatua ya mwisho na tutatoa taarifa,” amesema Bukumbi.
Aidha, amesema matukio ya jinai yanashuhulikiwa ipasavyo, huku akisema wamejipanga vizuri kushughulia matukio yote.
Hata hivyo, Amesema asilimia 90 ya matukio yanafanikiwa kutokana na ushirikiano uliopo baina yao na wananchi na kwamba matukio ya kihalifu yamekuwa yakipungua.
Awali, akizungumza katika mazishi ya Christina, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba alisema Serikali ipo kazini katika kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji hayo wanakamatwa.
“Tunafanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya mkoa pamoja na kupata msaada kutoka mikoa jirani, lengo letu ni kuwafikia wahusika kwenye mikono ya sheria,” amesema.
Ещё видео!