Mwa 14:18-20
Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.
Zab 110:1-4
Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako
Kuwa chini ya miguu yako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki
Bwana atainyosha toka Sayuni
Fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako;
(K) Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki
Watu wako wanajitoa kwa hiari,
Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki
Bwana ameapa,
Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki.
(K) Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki
1Kor 11:23-26
Mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
Yn 6:51
Aleluya, aleluya
Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni, asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele
Aleluya
Lk 9:11-17
Makutano walimfuata Yesu; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa. Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu. Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula. Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini. Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili.
Ещё видео!